Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Balozi Simon Sirro, ameagiza kufanyika uchunguzi wa haraka kubaini chanzo cha vifo vya samaki vilivyoripotiwa katika Mto Malagarasi, kijiji cha Kigadye wilayani Kasulu.
Akikagua eneo hilo akiwa na Kamati ya Usalama ya Mkoa na Wilaya, Sirro amewataka wananchi kuepuka kutumia samaki waliokufa kama kitoweo na pia kuwa waangalifu katika matumizi ya maji ya mto huo hadi matokeo ya uchunguzi yatakapobainishwa.
Afisa Usafi na Mazingira wa Mkoa huo, Nesphory Sungu, amesema sampuli za maji tayari zimechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu, huku akibainisha kuwa hadi sasa hakuna madhara yaliyothibitishwa. Aidha, amewasihi wananchi watakaopata changamoto za kiafya baada ya kula samaki hao kufika hospitalini mara moja kwa uchunguzi na matibabu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dkt. Damas Kayera, amethibitisha kuwa hakuna mgonjwa aliyeripotiwa kuathirika, lakini ameendelea kuwasihi wananchi kufika vituo vya afya haraka iwapo watapata dalili zozote zinazohusiana na matumizi ya maji ya mto huo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.