Na Waandishi Wetu
Imeelezwa kuwa Tanzania imeweza kufikisha miaka 60 ya Muungano kutokana na awamu zote za utawala kuwa na sera endelevu kwa kufuatilia kwa karibu changamoto zinazojitokeza na kuzipatia ufumbuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye ameyabainisha hayo leo wakati wa kilele cha maadhimisho ya sherehe ya miaka 60 ya Muungano ambayo kimkoa yalifanyika katika Uwanja wa Umoja wilayani Kasulu.
“Kupitia Muungano wetu sote ni mashahidi kwamba uchumi wetu umeendelea kuimarika siku hadi siku kutokana na mazingira na mahusiano mazuri yaliyowekwa na viongozi wetu,” amesema.
Aidha, Andengenye amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa amesema kuwa katika miaka 60 ya Muungano serikali imeweza kuimarisha huduma za afya kwa kuboresha miundombinu pamoja na kuwekeza katika vifaa tiba vya kisasa.
“Mkoa wa Kigoma kabla ya miaka 60 ya Muungano tulikuwa na vituo vya afya visivyozidi 11 lakini hivi sasa tuna vituo vya kutolea huduma hizo zaidi ya 230 vinavyojumuisha Hospitali ya Rufaa moja, hospitali za wilaya zaidi ya nane pamoja na vituo vya afya na zahanati zaidi ya 200,” amesema.
Awali akizungumza katika sherehe hizo Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu amesema katika miaka 60 ya Muungano kumekuwa na manufaa mengi ikiwemo kutokuwepo na ubaguzi wa mipaka baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.