Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu imekamilisha ujenzi wa nyumba tano za watumishi wa Afya zilizojengwa katika hospitali ya halmashauri hiyo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na kutoa motisha kwa watumishi hao kwa kuwapa makazi bora na salama
Nyumba hizo zilizogharimu kiasi cha shilingi Mil.290 zimejengwa kwa fedha zitokanazo na mapato ya ndani ya Halmashauri kwa awamu ya kwanza ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa nyumba bora za watumishi na kupunguza malalamiko katika utoaji wa huduma kwani watumishi walikua wakilazimika kutembea umbali wa kilomita 18 ili kufika katika Kituo cha kazi.
Akizungumzia ukamilishaji wa nyumba hizo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Dkt. Robert Nelson Rwebangira alisema kuanzia mwaka 2023 wananchi wategemee kupata huduma bora zaidi kwani watoa huduma watakuwa wakipatikana kwa urahisi kutokana na utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa nyumba bora za watumishi.
"Kilichotusukuma kujenga nyumba hizi ni kwa Kata za karibu Nyakitonto na Nyamnyusi ni ngumu sana kupata nyumba bora, lengo kuu la kujenga nyumba hizi ni kuhakikisha huduma za afya za dharula zinapatikana masaa yote 24 kwa muda muafaka watoa huduma watapatikana kiurahisi kushughulikia dharula kwa wakati lakini pia ni motisha kwa watumishi kuwapa makazi bora ambayo ni salama", alisema Rwebangira
Aliongeza kuwa kukosekana kwa makazi kwa watumishi wa kada hiyo kulikuwa kunaleta changamoto ya gharama kubwa ya utoaji wa huduma za dharula kwa wagonjwa pia malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwa kukosa huduma kwa wakati muafaka hivyo nyumba hizo zitasaidia kupunguza vilema na vifo kwa wanaopata ajali vilevile kuzuia vifo kwa wamama na watoto
Kwa upande wake Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Eng. Athanasi Nziganyije Msuta alimshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Ndugu Joseph Kashushura Rwiza kwa kujali na kuwapatia watumishi wa Idara ya Afya makazi bora na salama
Alitoa rai kwa wananchi wote wa halmshauri ya Wilaya ya Kasulu kuunga mkono shughuli zote za maendeleo zinazofanywa katika halmashauri hasa katika swala zima la ukusanyaji wa mapato ili kuleta maslahi mapana ya halmashauri na nchi kwa ujumla.
Halmashauri Ya Wilaya Ya Kasulu inatarajia kuendeleza ujenzi wa nyumba 4 za watumishi wa Idara ya Afya katika awamu ya pili zenye uwezo wa kubeba familia tatu katika kila nyumba na kutenga kiasi cha fedha shilingi 133,843,463.17 kwaajili ya ujenzi huo, nyumba za Wakuu wa Idara zote, kituo cha Polisi na nyumba za Polisi katika Kata ya Nyakitonto kupitia mapato ya ndani.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.