Na Mwandishi Wetu, Kasulu
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, Dkt. Semistatus H. Mashimba ametoa maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wilayani humo kwa kutumia mfumo unaoakisi 4R za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikisha makundi tofauti katika jamii.
Tukio hilo limefanyika leo Alhamisi Septemba 26, 2024 katika Ofisi za Makao Makuu ya Halmashauri hiyo eneo la Nyamnyusi na kuhusisha viongozi wa vyama vya siasa,viongozi wa dini,wazee maarufu,vyama vya wafugaji na wakulima,watendaji wa vijiji na kata pamoja na waandishi wa habari.
Akizungumza katika tukio hilo Dkt. Mashimba amesema kuwa ni takwa la kisheria lililomtaka kufanya hivyo ili wananchi wapate maelezo siku 62 kabla ya tarehe ya uchaguzi kwa lengo la kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa wapiga kura pamoja na wagombea kupata taarifa zote kwa wakati.
“kampeni zitaanza tarehe 20 hadi 26 Novemba 2024 na uchaguzi utakuwa Novemba 27 mwaka huu kwahiyo tuwaombe vyama vya siasa,viongozi wa dini na wadau wote mliopo hapa tunaomba kipindi hiki kiwe na utulivu na amani kubwa tofauti na mazingira mengine,” amesema.
Naye Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kasulu, Abdallah Kazikwa ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Mkazi ambalo ni tofauti na zoezi lililopita la uandikishwaji katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura ili waweze kuitumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowafaa.
Kwa upande wao viongozi wa vyama rafiki Wilaya ya Kasulu wameipongeza Kamati ya Uchaguzi kwa kuwashirikisha katika tukio hilo muhimu huku wakibainisha kuwa na imani nayo pamojana kutoa ahadi ya kuipa ushirikiano pale utakapohitajika.
Katika hatua nyingine Katibu wa Baraza la Machifu Mkoa wa Kigoma,Abel Bussa ametoa rai kwa kila mwananchi mwenye sifa kujitokeza kugombea pamoja na kutoa ahadi ya kwenda kufundisha aliyojifunza leo kwa wengine juu ya umuhimu wa kupiga kura.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.