Waheshimiwa Madiwani pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria, wakifuatilia jambo wakati Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Kasulu ukiendelea.
Na. Andrew Mlama
Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu robo ya tatu kwa mwaka 2017/2018, umefanyika leo ambapo viongozi mbalimbali toka vyama vya siasa, madhehebu ya dini, vyombo vya ulinzi na usalama, wananchi toka kata mbalimbali pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo wamehudhuria.
“Akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mh. Yohana Mshita, amewataka Madiwani kushirkiana na wananchi kwa ukaribu katika kusimamia maendeleo ili kuhakikisha Halmashauri inasonga mbele. “Hakikisheni mnawashirikisha wananchi na mawazo yao yafanyiwe kazi, hii itaamsha ari ya kujitolea katika utekelezaji wa shughuli za Maendeleo’’ alisisitiza Mshita.
Akijibu swali la Papo kwa papo lililoulizwa na Diwani wa Kata ya Bugaga Mh. Fidel Mtemwa ambapo alitaka kufahamu, Halmashauri inampango gani katika kuhakikisha bei za mazao zinapanda na kumnufaisha mkulima. Akijibu swali hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema suala hilo ni la kisera kwani linahusu nchi nzima.
“Serikali hairuhusu mazao ya chakula kuuzwa nje ya nchi mpaka ijiridhishe na kuhakikisha kinatosheleza Mikoa yote nchini. Upo mpango wa kujenga ghala kubwa la mazao wilayani hapa kwani wakulima huuza mazao wanayoyapata wakati wa mavuno kutokana na kukosa miundombinu mizuri ya kuhifadhia ili kuyauza baadae kwa bei yenye faida” alihitimisha Kasekenya.
Akichangia uwasilishwaji wa Taarifa ya Kamati ya Kupambana na kudhibiti UKIMWI, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya Bi.Victoria Makyao amesema ili Jamii iendelee lazima iwe na Afya njema. Suala la UKIMWI lizungumzwe katika Jamaii bila kificho. Wazazi wazungumze na watoto wao ili waweze kuchukua tahadhari dhidi ya UKIMWI.
Amewataka wananchi wawe makini kipindi hiki cha mavuno kwani kunamuingiliano mkubwa wa wageni toka mikoa mbalimbali wanaokuja kufanya biashara ya mazao. aidha amewakumbusha wakulima wa kasulu kutimimiza malengo yao mara baada ya kuuza mazao badala ya kujihusisha na masuala ya starehe.
Baraza la madiwani limepitisha pendekezo la eneo la Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, ambapo Wajumbe kwa pamoja walikubaliana eneo lililopo katika Kata za Nyamnyusi na Nyakitonto litumike. “Eneo hilo ni katikati kuendana na Jiografia ya Wilaya yetu pia linafikika kutoka kata zote zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu” alisisitiza Mh. Hosea Nyamwombo Diwani wa Kata ya Buhoro.
Wanachi waliohudhuria wamepongeza uendeshwaji wa Mkutano wa Baraza la Madiwani, wamesema kuwa Madiwani ambao ndio wawaakilishi wao wamechangia michango yao kwa weledi, kisha kujibiwa hoja zao kwa umakini. Hali hiyo imewapa Imani juu ya uendeshwaji wa shughuli za Kiserikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.