Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Mzee Mkongea Ali akijiandaa kupanda Mti mara baada ya kuzindua Klabu ya kupinga rushwa iliyopo Shule ya Sekondari Kimwanya.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Mzee Mkongea Ali akitoa maelekezo kwa Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Ndg. Issa Tangira kabla ya kuweka jiwe la msingi kwenye shule ya Msingi Kasasa ambapo umefanyika ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, Ofisi moja ya walimu na vyoo matundu sita.
Ndg. Mzee Mkongea Ali akikagua msitu wa Kijiji cha Kalimungoma kilichopo kata ya Makere. Msitu huo wenye ukubwa wa zaidi ya Ekari 150 unamchanganyiko wa Miti mbalimbali ya Asili iliyohifadhiwa pia unatumika kwa ajili ya ufugaji wa Nyuki.
Muonekano wa shamba la mfano la Kilimo cha Pamba lililopo Katika kijiji cha Kalimungoma katika kata ya Makere ambalo limetembelewa na kukaguliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Mzee Mkongea Ali.
Baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Kasulu (kutoka Kushoto) Mwenyekiti wa CCM (W) Ndg. Mbelwa Abdallah Chidebwe, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange, Mkurugenzi Mtendaji (W) Kasulu Mhandisi Godfrey Kasekenya, Mh. Vuma Hole Mbunge wa Kasulu vijijini, Ndg. Mashaka Mshola ambaye ni Katibu wa CCM(W) Kasulu na Mh. Yohana Mshita, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu wakimsikiliza Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Mzee Mkongea Ali wakati akitoa Ujumbe wa mbio za Mwenge kwa wananchi waliojitokeza kuupokea Mwenge wa Uhuru kwenye kata ya Makere.
Hongera Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ndg. John Joseph Pombe Magufuli, Hongera kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu kwa kuendelea kusimamia utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambayo ni chachu ya Maendeleo kwa Taifa. Ndivyo inavyosema Taswira ya picha hii ikionesha baadhi ya wakazi wa kata ya Nyamidaho wakijielekeza kuupokea Mwenge wa Uhuru.Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu Mha. Godfrey Kasekenya (Kulia) akitoa ufafanuzi wa jambo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ndg. Mzee Mkongea Ali.
Na. Andrew Ginnethon.
Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2019 zimefanyika wilayani hapa ambapo zimezindua, kuweka jiwe la msingi pamoja na kutembelea Miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Mbio hizo zimefanyika leo Tarehe 21.4.2019 ambapo jumla ya miradi Sita yenye Thamani ya Shilingi 623,097,600 imetembelewa. Kati ya miradi hiyo mitatu imekaguliwa, mmoja umezinduliwa, mradi mmoja umewekewa jiwe la msingi. Hata hivyo mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Nyamidaho haukuweza kuzinduliwa kutokana na uwepo wa dosari ndogo za kiufundi ambapo imeagizwa yafanyike marekebisho ndani ya muda mfupi.
Akitoa ujumbe wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2019 kiongozi wa mbio hizo Ndg. Mzee Mkongea Ali ameitaka jamii kuepuka matumizi ya madawa ya kulevya, kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, kuendeleza mapambano dhidi ya Rushwa, kutokomeza Maralia na kupambana na ugonjwa wa UKIMWI.
Ndg. Mkongea amesema kuwa, Sekta ya Maji ni muhimu sana kwa maisha ya binadamu. Kupitia Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, Serikali itahakikisha Wananchi wote wanaoishi vijijini wanapata maji safi na salama kwa asilimia 85 na wale wa wanaoishi mijini wanapata asilimia 95 ifikapo mwaka 2020.
Amesisitiza Wananchi kuacha kufanya shughuli mbalimbali za kibinaadamu kama Kilimo, kulisha mifugo pamoja na kujenga katika vyanzo vya Maji. Aidha ametoa Rai kwa wananchi kutoa taarifa kwenye vyombo vya Sheria pale wanapoona kuna mtu anatekeleza shughuli za kibinaadamu katika maeneo yenye vyanzo vya Maji.
Mkongea amewataka wananchi wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu kuhakikisha wanashiriki uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ifikapo mwezi Oktoba 2019. “Chagueni kiongozi atakayewahakikishia analeta maendeleo, yeyote mwenye sifa asisite kujitokeza na kugombea na baada ya uchaguzi toeni ushirikiano mzuri kwa watakao shinda katika chaguzi hizo ili tujenge taifa” amesisitiza Ndg. Mkongea.
Akisoma Risala ya utii kwa Mhe. Rais, Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu Ndg. Titus Mguha amesema utekelezaji wa miradi ya Maendeleo iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019 umefanikishwa na Serikali kwa kushirikiana wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo. Miradi yote inajumla ya Shilingi 623,097,600 ambapo Fedha kutoka Serikali kuu ni Sh. 500,000,000 sawa na asilimia 80, Halmashauri ikichangia Sh. 7,353,000, sawa na asilimia 1, michango ya Wananchi Sh. 41,076,000 sawa na asilimia 7 na wahisani ikiwa Sh. 74,668,600 sawa na asilimia 12.
Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 Serikali kuu inatekeleza miradi mipya mine yenye Thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni tano ya vijiji vya Titye, Nyamnyusi, Kitema na Kitagata ambapo tayari imetangazwa kwa ajili ya kupata wakandarasi. “Miradi hiyo ikikamilia, itaongeza ubora katika huduma ya upatikanaji wa Maji kwa asilimia 5.4 sawa na watu 27,960.’’amesema Mguha.
Mbio za Mwenge wa Uhuru zimehitimishwa katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu ambapo zitaendelea wilaya ya Kibondo mkoani hapa.
Mwenge wa uhuru mwaka 2019, umebeba Kauli mbiu isemayo “Maji ni Haki ya kila Mtu, Tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.