Katibu Tawala ya Wilaya ya Kasulu Titus Mghuha amewataka viongozi ya Kata na vijiji kuwasaka wanafunzi waliopo katika Kata zilizopo kwenye Mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa MEMKWA
Aliyasema hayo wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya siku tano ya walimu wa MEMKWA, iliyohusisha walimu wakuu na maafisaelimu wa kata tano za halmashauri ya wilaya ya Kasulu yaliyofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Ualimu Kasulu.
Mghuha alisema kuwa, pamoja na ufadhili uliotolewa ili kuutekeleza mpango huo, sio jambo la kujivunia kuuona mkoa wa Kigoma ukiwa na idadi kubwa ya watoto zaidi ya elfu thelathini waliokosa elimu ya msingi.
“Kupitia mafunzo haya viongozi wote wa kata na vijiji nawaagiza kuwasaka watoto wanaostahili kujiunga na mpango wa Elimu ya Msingi Kwa Waliokosa na kuwapeleka shule ili baada ya miaka mitano, mkoa wa Kigoma usiwe na historia hiyo,” alisema Mghuha
Kwa upande wake Afisa Elimu ya Watu Wazima mkoa wa Kigoma Hawamu Tambwe alisema kuwa mpango huo wa kuwapatia watoto elimu nje ya mfumo rasmi, utatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na kuzihusisha halmashauri zote za mkoa wa Kigoma.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, jumla ya watoto 32,564 wenye umri wa miaka 9-16 watahusika kati yao wavulana wakiwa 15,420 na wasichana 17,144.
"Kupitia mpango huo, watoto 4,959 wanatarajiwa kurudishwa shuleni mwaka wa kwanza, watoto 6,024 watarudishwa shuleni mwaka wa pili, watoto 6,408 watarudishwa shuleni mwaka wa tatu, watoto 7,165 watarudishwa shuleni mwaka wa nne huku watoto 8,008 wakitarajiwa kurudishwa shuleni katika kipindi cha mwaka wa mwisho wa mpango huo", amesema.
Akizungumza katika hafla hiyo, mwakilishi wa Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia Elimu ya Watu Wazima Godliver Nkala, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha watoto walio nje ya shule, wanaingizwa katika mpango huo.
Aidha kupitia kikao hicho, Nkala amepigilia msumari suala la chakula cha mchana shuleni kwa kuwataka washiriki wa mafunzo hayo kuihamasisha jamii katika kushiriki kikamilifu kufanikisha ajenda hiyo.
Miongoni mwa washiriki wa siku ya mwisho ya mafunzo hayo ni Watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na wenyeviti wa vijiji kutoka katika kata tano zilizo kwenye mpango huo.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.