Imeandaliwa na Waandishi Wetu
Imeelezwa kuwa Wilaya ya Kasulu imepiga hatua kubwa katika eneo la uwekezaji hivi sasa baaada ya kuwa na usalama wa kutosha,suala la nishati hasa ya umeme pamoja na uhakika wa upatikanaji wa rasilimali watu.
Hayo yamebainishwa jana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Isaac Mwakisu kwenye sherehe za maadhimisho wa Miaka 62 ya Uhuru kwa ngazi ya wilaya ambapo alikuwa mgeni rasmi.
Amesema masuala hayo matatu yamesaidia kupata wawekezaji wakubwa wakiwemo wale wa kiwanda cha Mufindi Papers au Kasulu Sugar waliopo eneo la Mkuyuni wenye shamba la miwa hekta elfu 40 chenye uwezo wa kuzalisha Sukari tani laki 3 kwa mwaka .
“Kiwanda hiki pia kitakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme kutoka katika miwa hiyo ambayo wataingiza katika Gridi ya Taifa pamoja na kutengeneza karatasi zinazoweza kutengeneza fedha na serikali kuziuza nje ya nchi," amesema.
Pia, amebainisha kuwa kutokana na uwepo wa mchakato wa uanzishwaji wa kiwanda cha Saruji ana uhakika kitaenda kuondoa kadhia ya upatikanaji wa bidhaa hiyo kwa gharama kubwa wilayani humo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Wilaya ya Kasulu akifunga maadhimisho hayo aliwashukuru washiriki kwa kutoa mada na kuchangia mijadala mbalimbali ambayo imesaidia kuongeza upeo wao wa uelewa.
“Mmefanya uwasilishaji mzuri ambao umeibua mijadala mbalimbali ambayo imeweza kuleta uelewa kwa washiriki katika siku hii ya leo mimi niseme niwashukuru sana kwa ushiriki wenu tuombe tu Mungu atuweke hai kwa ajili ya tarehe 9 Desemba hapo mwakani," amebainisha.
Awali akizungumza katika maadhimisho hayo Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kasulu,Athumani Issango aliwahakikishia washiriki kuwa jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua askari yeyote atakayetoa lugha chafu kwa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.
Naye Kamnda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wa wilaya hiyo,Nathanae Mdegela aliwataka wanasiasa na mawakala wao kuelekea katika uchaguzi mwakani kushirikiana nao kupambana na vitendo vya rushwa ambavyo huwa vinashamiri inapofika kipindi hicho.
Sherehe hizo zilipambwa na mada mbalimbali za ukatili wa kijinsia, mapambano dhidi ya rushwa,hatua ya maendeleo tulipotoka, magonjwa yasiyoambukizwa na shughuli za kijamii kwa Jeshi la Magereza kwa ajili ya wafungwa.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.