Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma inategemea kutumia kiasi cha bilioni 39 fedha za Kitanzania katika kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019.
Hayo yamebainika katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kasulu kilichofanyika hivi karibuni kupitia kupitia maksio ya mpango wa bajeti ya halmashauri hiyo.
Akiongea, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Kasulu, Mheshimiwa Said Ndiyunze amesema kuwa changamoto za kushuka kwa bei za mazao ya chakula zinaonyesha namna shughuli za kilimo zinavyofanikiwa wilayani humo.
Taarifa ya mapitio ya bajeti iliyowasilishwa katika kikao hicho, imebainisha vipaumbele vya halmashauri hiyo kuwa ni uboreshaji wa ufaulu wa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, uimarishaji wa kilimo, kuongeza ukusanyaji mapato na kuboresha mazingira ya kazi na watumishi.
Katika juhudi za kutekeleza vipaumbele hivyo, baraza hilo la madiwani limepitisha maombi maalumu ya sh. bilioni 4.6 zitakazotumika kununua magari manne kwa ajili ya matumizi ya Mkurugenzi wa halmashauri, Idara ya mipango, na idara mbili za elimu msingi na sekondari.
Malengo mengine ya maombi ya fedha hiyo ni ujenzi wa miundombinu ya hospaitali ya wilaya na kupunguza deni la shilingi bilioni 2 wanazodai wazabuni na wakandarasi wa halmashauri yenyewe.
Aidha, baadhi ya waheshimiwa Madiwani walionesha wasiwasi kuhusu uhalisia wa makisio ya bajeti iliyowasilishwa kutokana na kuporomoka kwa bei za mazao, ikilinganishwa na kipindi yalipofanyika makisio hayo.
"Tulitarajia mapato ya ndani ya kutosha kutokana na ushuru na tozo za mazao, lakini kutokana na wingi wa mavuno baadhi ya mazao bei zimeporomoka huku zao la tumbaku likikosa wanunuzi, hali hii itakwamisha malengo yetu." Alisema diwani wa Rungwempya, Mh. Jonas Abel.