Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, yapongezwa kwa kwa kupata hati safi na kupunguza idadi kubwa ya hoja hadi kufikia tarakimu moja kwa kuwa na hoja tisa kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Ikiwa ni mara ya nne mfululizo,maafanikio hayo yameiletea heshima si tu halmashauri hiyo, bali pia mkoa mzima wa Kigoma.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Juni 16, 2025, na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye, wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani kupitia na kujadili hoja za CAG uliofanyika katika Ukumbi wa Kagoma, makao makuu ya halmashauri.
“Nawapongeza Mwenyekiti wa Halmashauri, Makamu wake, Mbunge wa Kasulu Vijijini, madiwani wote, Mkurugenzi na wataalamu kwa kazi nzuri iliyowezesha halmashauri kupata hati safi katika ukaguzi wa CAG kwa mwaka ulioishia Juni 2024. Hongereni sana,” amesema Kanali Ngayalina.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufunga hoja zote zilizosalia kwa vielelezo na kutekeleza maagizo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC). Akieleza kuwa lengo la mkoa ni kuhakikisha hoja zote zinapungua hadi kufikia tarakimu moja ifikapo mwaka wa fedha 2025/2026.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mhe. Eliya Kagoma, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri baina ya madiwani, wataalamu, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, vyombo vya ulinzi na usalama, Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Naye Mkaguzi Mkuu wa Nje kutoka Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Honest Muya, ameitaka halmashauri kushughulikia changamoto ya watoto kushindwa kusoma. Ameahidi kuwa ofisi yake itaendelea kutoa ushauri elekezi kuhusu namna bora ya kushughulikia tatizo hilo katika mwaka wa ukaguzi unaofuata.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.