Na Mwandishi Wetu, Kasulu
Jumuiya za Kujifunza kwa Walimu Wakuu na Maafisa Elimu Kata (JZK) zimelenga kuwajengea uwezo viongozi wenye mamlaka kwenye mazingira wanayoyaongoza ili waweze kufikia malengo ya Dira ya Elimu ya Taifa ya Mwaka 2025.
Hayo yamebainishwa leo wilayani Kasulu na Mwezeshaji Kiongozi, Japhet Kidawi wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu ya JZK kwa maafisa elimu kata na walimu wakuu wa halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yanayofanyika katika Chuo Cha Ualimu Kabanga.
“Mafunzo haya yanatolewa kupitia Mradi wa Shule Bora ambao una afua mbalimbali zikiwemo ujifunzaji na ufundishaji ambapo JZK inapatikana humo ,” amesema.
Ameongeza : “inayolenga kumpa uwezo kiongozi ambaye ni msimamizi ili kufikia malengo ya Dira ya Elimu ya Mwaka 2025 inayosisitiza elimu bora na jumuishi inayolenga kumbadilisha mtu aweze kubuni, kujitambua,kuhoji,kudadisi,kupenda kazi na kuwa na mwenendo unaostahili,” ameeleza Kidawi.
Naye Afisa Elimu Taaluma Msingi wa Halmashauri hiyo,Joseph Maiga amesema kuwa lengo kubwa la mafunzo hayo ni kubaini changamoto zinazotoka shule moja kwenda nyingine kuona ni namna viongozi wa elimu wa maeneo hayo watakavyosaidiana kuzitatua.
“Unaweza kukuta katika Kata moja kuna shule kumi huku tano ndio zinafanya vizuri sana kwenye ufaulu kwahiyo wanapokutana viongozi wa elimu wanaweza kupeana uzoefu kwa wale ambao hawafanyi vizuri ili nao waongeze ufaulu,” amesema.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Kata ya Kwaga, Rebeca Bitebu amesema kuwa Kupitia mafunzo hayo amepata ujuzi mpya hasa kwenye suala zima la utatuzi wa changamoto za suala zima la usimamizi na ujifunzaji kwenye elimu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA KASULU
Anuani ya Posta: S.L.P 97
Simu ya Mezani: +255-028-2810339
Simu: +255-028-2810339
Barua Pepe: ded@kasuludc.go.tz
Copyright ©2024 kasuludc . All rights reserved.